KUANDAA MPANGO WAKO WA 2017 –USIKOSE:

KUANDAA MPANGO WAKO WA 2017 –USIKOSE: Wakati tunakaribia mwisho wa Mwaka 2016 na kutakiana heri ya mwaka mpya ni vyema tukajipanga kwa ajili ya mwaka 2017. Lakini kabla ya kujipanga kwa mwaka mpya inabidi kujipima mafanikio na changamoto tulizokutana nazo mwaka 2016. Maswali yafuatayo yatakusaidia katika kujipima:
1. Je uliweza kufikia malengo yako ya kimaisha (kishule, kikazi, kibiashara na kifamilia)?
2. Ni mambo gani unajivunia kuyatimiza mwaka huu wa 2016 na ni yapi yaliyobaki?
3. Umejifunza nini katika mwaka wa 2016 na utatumiaje elimu hiyo kuboresha utendaji wako na kazi unayoifanya kwa mwaka ujao?
Baada ya kujibu maswali hayo sasa chukua kalamu yako na karatasi na andaa mpango wako rahisi kama ifuatavyo:
1. Mazingiza ya biashara, kazi au shule: Katika kuelewa hali halisi ni vyema ukapima mabadiliko makubwa yaliyotokea mwaka huu wa 2016 na kuangalia jinsi yanavyoweza kuathiri utendaji wako au kuwa fursa. Kwa mfano sasa tuna serikali mpya ambayo imekuja na mambo mengi mapya:
• Ulipaji wa kodi sasa umeengezeka
• Serikali imepunguza wafanyakazi hewa na wanafunzi hewa
• Kumekuwa na msisitizo wa kufanya kazi
• Safari za nje zimepunguzwa
• Bajeti ya serikali imeelekezwa zaidi kwenye uwekezaji
• Serikali imeanza mpango wa kuhamia Dodoma
• Serikali inabana matumizi
• Serikali inaweka msisitizo katika ujenzi wa viwanda
• Kuna kodi mbalimbali mpya zilizoanzishwa n.k
Mabadiliko hayo na mengine mengi yanaweza kuwa ni fursa kwako au changamoto. Mfano kama serikali inajenga Dodoma na kuoengeza uwekezaji ni fursa gani zipo? Au ni changamoto gani zipo katika mradi wako au mambo yako?
2. Baada ya kupima mazingira ni vema sasa ukaweka dira yako ya kikazi, kibiashara au kielemu. Anza kwa kuandika dira yako ya mwaka kwa maana ya unataka kuwaje mwisho wa mwaka 2017 au unataka mradi wako au biashara yako iweje mwisho wa mwaka. Andika dira yako sasa.
3. Baada ya dira yako andika malengo yako. Lengo lazima liwe mahususi, liwe na muda maalum, liwe linafikika na unaweza kupima matokeo yake (Specific, Measurable, Achievable, Relevant and Time Frame –SMART Objective). Kwa mfano: Kwa mwaka 2017 nitaongeza mauzo ya biashara yangu kwa asilimia 20. Kwa 2017 nataka niongeze kiwango changu cha ufaulu kwa asilimia 30. Unaweza kuwa na melengo mengi tu kwa kuongozwa na dira yako. Sasa chukua kalamu yako andika malengo yako.
4. Andika mikakati itakayokuwezesha kufikia malengo yako. Kwa mfano ili kuongeza mauzo utafanya nini? Unaweza kuonyesha mbinu mbalimbali kama kuongeza matangazo kwa njia ya mtandao, kutembelea wateja zaidi, kuboresha huduma, kufikia masoko mapya n.k. Sasa andaa jedwali lenye malengo na mikakati ya kufikia kila lengo. Katika kila mkakati onyesha mhusika.
5. Andaa vipimo vyako (target zako) katika kufikia malengo- Kwa mahususi kabisa hakikisha unaonyesha target za jumla katika shughuli yako na za kila mmoja. Mkiwa zaidi ya mmoja katika shughuli, hakikisha kila mtu anawekewa target yake na mkubaliane jinsi ya kuifikia.
6. Weka mfumo wa kupima ufanisi na jinsi utakavyompima kila mmoja katika kazi au kijipima mwenyewe katika kazi yako au katika elimu au kitu chochote unachokifanya.
7. Kama kuna gharama mbalimbali au rasilimali (resources) zitakazohitajika hakikisha unaziandika zote ili uweze kuafanya utaratibu wa kuzipata.
Hakikisha unafanya mambo niliyokushauri yatakusaidia kuwa na mpango rahisi wa mwaka. Usiwe kama watu wengi wanaoanza mwaka bila mpango wowote. Muhimu kuliko yote ukipanga kufanya kitu kifanye. Ukizingatia haya utaona tofauti kubwa na kama utafanikiwa usiache kunitaarifu.

Dr. Goodluck Urassa
Mkurugenzi wa EFL