MWANZO WA KUDUMAA AU KUANGUKA KWA BIASHARA.

MWANZO WA KUDUMAA AU KUANGUKA KWA BIASHARA.
Biashara nyingi zimekuwa zikifa muda mfupi tu baada ya kuanzishwa kutokana na sababu ambazo kimsingi mfanya biashara anatakiwa kuwa makini nazo pindi anapo hitaji kuanzisha biashara au afanyapo biashara. Kwa leo, tuangalie mambo muhimu matatu ya kuzingatia ili biashara yako iwe yenye Mafanikio.

1. Anzisha biashara yenye kutatua matatizo ya watu na iwe kwenye eneo sahihi. Mfano mzuri ni pale unapo fungua biashara ya kuuza vocha na huku mtandao haupo eneo husika au kama upo unasuasua sana na umepoteza mvuto kwa wateja. Ni dhahiri kuwa hizo vocha unazo uza zitakosa wateja na huko kunakuwa ni kupoteza muda na pesa pia, na ndivyo ilivyo hata kwa biashara zingine ukikosea kuanzisha biashara ambayo haitatui changamoto za watu wa eneo husika ni rahisi sana kudumaa na mwishowe inakulazimu uifunge.

2. Usimamizi mbovu na kukosa uvumilivu.Mara nyingi wanao achiwa biashara ili wazisimamie hushindwa kuendana na matakwa na matarajio ya mhusika.Umakini wa kuchagua msimamizi wa biashara yako aliye sahihi ndio jambo la msingi zaidi.Pia unatakiwa kuwa mvumilivu katika biashara yoyote ile. Ipe muda biashara yako , fanya matangazo , biashara yako ikifahamika utapata mafanikio unayo yahitaji. Wafanyabiashara wengine hukosa subira na kutokana na haraka zao hujikuta wanaua mtaji na kufunga biashara zao kwa kukimbilia mafanikio ya haraka.

3. Kufanya biashara na watu wasio sahihi. Tafuta mtu sahihi wa kufanya nae biashara, lazima kuwepo na malengo yanayo waunganisha na yenye maslahi baina ya pande zote. Mfano kuna mtu mwingine unamtumia pesa akuagizie mzigo lakini kwa kuto kujali kwake , mzigo unachelewa na haufiki kwa wakati,mwishowe anakutumia bidhaa muda anaotaka yeye. Hivyo basi ni muhimu uwe na watu sahihi watakao kufanya ufikie matarajio yako.