
Enterprise Finance Limited (EFL), kwa kushirikiana na BUMACO INSURANCE, AKILI SOFT, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na IMED, imeendesha Semina ya Uwekezaji na Biashara iliyolenga kuwajengea washiriki ujuzi wa ujasiriamali, uongozi, uwekezaji, bima na afya ya akili kwa ajili ya kukuza biashara na kuimarisha ustawi wa kiuchumi.
Semina hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba Mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), iliwakutanisha washiriki 550 kutoka makundi mbalimbali, yakiwemo wafanyabiashara binafsi, wawakilishi wa makampuni na wafanyakazi kutoka sekta tofauti.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na wawezeshaji wanne waliotoa maarifa katika maeneo muhimu yanayochangia maendeleo ya biashara na ustawi wa mtu binafsi.

Akizungumza kuhusu ujasiriamali, uongozi na kujenga mkakati wa kukuza biashara, Prof. Goodluck Urassa alisisitiza umuhimu wa kujikita katika ujasiriamali, kujiwekea malengo yanayopimika na kuyafuatilia kwa nidhamu ili kufikia mafanikio yanayotarajiwa. Alieleza kuwa ukuaji wa biashara unahitaji mipango madhubuti, uongozi bora, utambuzi wa fursa na utekelezaji wa mikakati endelevu.
Aidha, Prof. Urassa alisisitiza kuwa EFL imekuwa zaidi ya Taasisi ya kifedha kutokana na juhudi zake za kurudisha kwa jamii kupitia utoaji wa elimu na maarifa yanayochangia maendeleo ya kiuchumi kila mwaka.
Alibainisha kuwa semina hizo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau mbalimbali, kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo wa kutumia fursa zilizopo kukuza biashara na kuboresha maisha yao.

Kwa upande wake, Mkurugeni wa BUMACO Dkt. Shirumisha Kwanyu aliwasilisha mada kuhusu bima na biashara, akieleza namna bima inavyochangia ustawi wa jamii na kusaidia biashara kukabiliana na changamoto na majanga yasiyotarajiwa. Alisisitiza umuhimu wa uelewa wa bima katika kulinda mali, kupunguza athari za kifedha na kuimarisha mwendelezo wa shughuli za biashara.

Naye Bw. Edmund Munyagi, akiwasilisha mada kuhusu uwekezaji katika masoko ya fedha na mitaji, alieleza namna watu wanavyoweza kutumia fursa za uwekezaji kujenga akiba na kukuza mali zao. Mada hiyo ilisisitiza umuhimu wa kuwa na mipango ya kifedha, kuweka akiba kwa utaratibu na kufanya maamuzi ya uwekezaji yanayozingatia malengo ya muda mfupi na mrefu.
Katika mada ya afya ya akili na biashara, Dkt. Kweka alizungumzia uhusiano kati ya afya ya akili, hisia na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika shughuli za biashara. Alieleza umuhimu wa kusimamia hisia na kukabiliana na shinikizo ili kuboresha maamuzi, kuimarisha mahusiano ya kikazi na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa biashara.
Kwa ujumla, mada hizo ziliweka msisitizo kwamba mafanikio ya biashara yanahitaji kuunganisha ujuzi wa ujasiriamali na uongozi, mipango ya uwekezaji, ulinzi wa kifedha kupitia bima na utunzaji wa afya ya akili.
Kupitia semina hiyo, EFL na washirika wake wameendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano katika kuimarisha elimu ya biashara na fedha kwa jamii, hususan kwa wafanyabiashara wanaohitaji maarifa na mikakati ya kukabiliana na changamoto za soko na kutumia fursa za kiuchumi.
Mpango huo unaendana na dhamira ya EFL ya kukua pamoja na wateja wake kwa kuwawezesha kupata maarifa na ujuzi unaoweza kuwasaidia kuanzisha, kusimamia na kukuza biashara zao kwa mafanikio.
Kaulimbiu ya EFL, “Growing with Your Enterprise”, inaakisi dhamira hiyo ya kushirikiana na wafanyabiashara katika safari yao ya ukuaji, huku ushirikiano na BUMACO INSURANCE, AKILI SOFT, UDSM na IMED ukiimarisha nafasi ya wadau mbalimbali katika kuchagiza maendeleo ya biashara na ustawi wa jamii.