- October 23, 2023
- Posted by: admin
- Categories: CSR, Events, News
Enterprise Finance Limited (EFL) ambayo ni Kampuni inayojishughulisha na kutoa huduma za fedha kwa wafanyabiashara na wafanyakazi imekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma mbalimbali za jamii katika maeneo mbalimbali ya nchi. Kama sehemu ya huduma zake kwa jamii, Kampuni hii imekuwa ikitoa elimu ya ujasiriamali na uwekezaji, ikiandaa na kuhamasisha wananchi kushiriki katika mazoezi na michezo mbalimbali kama vile kucheza mpira na kukimbia, na pia kuchangia vifaa vya kufundishia katika shule mbalimbali.
Kama sehemu ya kusherekea mwezi wa huduma kwa wateja, ambao Kampuni hii imekuwa na utaratibu wa kufanya hivyo kila mwezi wa kumi, mwaka huu imejikita katika kushiriki kweye usafi na kutunza mazingira. Akizungumza leo tarehe 21 Oktoba 2023, wakati viongozi na wafanyakazi wa EFL wakishirikiana na wananchi wa Kawe kusafisha fukwe za bahari katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa EFL Bi. Jacqueline Lujuo alilieleza gazeti hili kuwa Kampuni yake imejipanga kuboresha mahusiano na jamii kwa kuelekeza nguvu katika suala la kutunza na kusafisha mazingira. Alieleza kuwa, EFL imeanza mkakati huu wa kutunza mazingira kwa muda mrefu ikishrikiana na taasisi nyingine katika kupendezesha maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam. Hivyo basi, leo tuko hapa kwenye Fukwe za Kawe kuondoa plastiki na taka nyingine hatarishi kwenye fukwe ili kuokoa maisha ya viumbe hai baharini, alieleza. Kwa kufanya hivi, tunalenga kuongeza ushawishi kwa jamii kusafisha na kutunza mazingira, alisema.
Naye, Profesa Goodluck Urassa, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya EFL, alitoa wito kwa wananchi wa maeneo hayo kuhakikisha wanazitumia fukwe za bahari na kuziacha katika mazingira safi kwa kuwa usafi wa mazingira ni wajibu wetu sote. Vile vile alisisitiza kuwa EFL itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na wanaharakati wa mazingira katika kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya kujenga utamaduni wa usafi katika jamii yetu.
Akifunga zoezi hilo, Profesa Urassa alisema kuwa Kampuni yake imekusudia kuendelea kuliwekea mkazo suala la kutunza mazingira maana mafanikio ya EFL yanaambatana na wajibu wa kuisaidia jamii kwa utaratibu endelevu. Alitoa wito kwa jamii na taasisi nyingine kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kutunza mazingira na afya za watu.
Kipekee aliwashukuru wadau wa mazingira wakiwa ni pamoja na NEMC, Manispaa ya Wilaya Kinondoni, makundi ya usafi, wanaanchi wa Kawe na vyombo mbalimbali vya habari kwa kuhakikisha zoezi la usafi linafanyika vizuri. Aliwakaribisha kushirikiana na Kampuni yake katika juhudi kama hizo. Pamoja na hayo aliahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii na wadau mbalimbali wa Kampuni hii.