- October 15, 2024
- Posted by: admin
- Categories: Events, News
Enterprise Finance Limited (EFL) imetoa semina ya uwekezaji na usimamizi wa fedha kwa makundi ya watu waliojiajiri na walioajiriwa kwenye biashara,lengo ni kuwezesha washiriki kujua njia bora za kuwekeza kwenye biashara na masoko.
Akizungumza katika semina hiyo iliyofanyika jijini Arusha Oktoba 5 mwaka huu, Mmoja wa wawezeshaji Prof.Goodluck Urassa ambaye ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa EFL anasema mafunzo hayo ni sehemu ya kusaidia jamii kuwekeza katika vyanzo vya uhakika wa kipato na kukuza uwekezaji.
“Katika mafunzo haya tunaangalia mambo mengi ikiwemo jinsi ya kusimamia Miradi ya uwekezaji na biashara pamoja na kuwekeza kwenye biashara na masoko ya fedha hasa katika vyanzo vya kipato tulivu” anasema Urassa
Kwa upande wake meneja wa kampuni hiyo Mkoani Arusha Hekima Adam amepongeza washiriki wa semina hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kupata elimu sahihi ya usimamizi wa fedha ambayo itakwenda kutatua changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara wengi.
“Washiriki wa semina hii wametoka sehemu mbalimbali hapa nchini wakiwemo washiriki kutoka Arusha, Dar es salaam, Dodoma na maeneo mengine,tunaamini elimu waliyoipata itawezesha biashara zao kukua badala ya kudumaa kutokana na elimu ya fedha waliyoipata” anasema Adam
Naye mshiriki wa semina hiyo kutoka Arusha mfanyabiashara mashuhuri Bi.Viola Milunga ambaye anafanya biashara ya kuuza mashamba na magari amewasihi wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kwenye semina zinazoandaliwa na EFL kwakuwa zinakwenda kuwapa wigo mpana wa kibiashara ikiwemo usimamizi mzuri wa Miradi
Semina hiyo imefadhiliwa na EFL kwa kushirikiana na BUMACO insurance pamoja na UTT-Amis.